MAMBO KAMA YALIVYO NJE YA TANZANIA

Tuesday, 4 October 2011

KAZI NA MAISHA NJE YA BONGO

14:12 By Mindset

Ninaanzisha mjadala ili yeyote yule mwenye kuweza kuchangia achangie kuhusu maisha na kazi nje ya bongo.

Kwa mtazamo wangu na baada ya kuzungumza na baadhi ya wadau ninaowajua waliopo nje ya bongo kwa sasa ni kuwa wengi huwa tuna mtazamo na matarajio makubwa sana tunapofikiria maisha na kazi nje ya bongo.

Si ajabu wengi wetu kufikiria kuwa mtu akiwa nje ya bongo, basi 'anakula bata'. La hasha, maisha popote ni mapambano japo raha ni sehemu ya maisha ila tukumbuke shida pia zipo hasa unapokuwa nchi jirani. Kuna wabongo ninaowajua wapo hapa Sauzi, wana hali mbaya ajabu mpaka unajiuliza kwanini hivi.

Mfano, sio rahisi kupata kazi nzuri ya ofisi unapokuwa nje ya bongo, labda uwe uliipata ukiwa bongo, na wakati mwingine vikwazo vinakuwa aina ya elimu uliyosoma bongo, mahitaji ya kitaaluma ya nchi husika, na lugha ya ndani inayotumika mfano kufanya kazi kama sales executive katika nchi za kiafrika, Asia au za ulaya ambapo english sio lugha kuu inayotumika.

Pia ikumbukwe kuwa tatizo la ajira lipo kila nchi na kila serikali ingependa kuona raia wake kwanza wanapata ajira kisha wageni.

Kuna aina ya ajira ambazo katika nchi nyingi huwa sio ngumu saana kupata kama vile kazi za kuhudumia wagonjwa, kuhudumia hoteli au katika migahawa,  kazi za usafi, kazi za mauzo kwa maduka (nchi nyingi zilizoendelea zina supermarkets na malls kibao), uhudumu katika vituo vya kuuza mafuta na kazi za kufundisha .
Isitoshe, hata ukipata kazi hizo gharama za maisha ya sehemu husika zinakuhitaji kuwa muangalifu kwa matumizi wakati huo ukijua una majukumu kibao pande za bongo. Wakati huu unaishi maisha yako yote kamili nchi jirani yaani chakula, mavazi, kulala, mapumziko (burudani) na kadhalika vyote vinahitaji fedha na baada ya gharama hizo inabidi uwe na akiba ya kusaidia pande za bongo kama ambavyo wengi uliowaacha bongo watakavyokutarajia wakati hawajui hata gharama zako za maisha na kiasi chako cha mapato.

Uzuri wa kipato cha nje ya bongo, ni kuwa chaweza kuonekana ni kikubwa katika mlinganisho wa kubadilisha fedha za kigeni kwenda za kitanzania. Hivyo wengi wanafanikiwa kutuma fedha bongo hata kama kipato chao ni kidogo kwani wakizichanga changa kwa muda fulani, kwa msaada wa exchange rate, kiasi cha fedha kinaonekana cha kuridhisha.

Kwa mazingira ya bongo na nje ya bongo, sehemu nyingi za nchi zilizoendelea zina muonekano wa kuvutia na hata miundo mbinu ni poa. Hii ni sababu nyingi ya kuonekana kuwa maisha ya nje ya bongo ni poa.

Hata hivyo maisha yanaweza kuwa poa ukipata kazi nzuri, mshahara mzuri na ukawa na nidhamu ya matumizi, waweza fanya mambo mengi ya maendeleo ndani ya bongo.

Nyumbani ni nyumbani, pamoja na uzuri wa baadhi ya mazingira ya nje ya bongo, maendeleo ya kiteknolojia, na maisha kwa ujumla, bado kuna mambo ambayo tukiwa nje ya bongo tunayamisss kama vile uhuru wa kufanya kazi, kutembea na vibali kila mahali, na baadhi ya kazi huwezi pata, bila kusahau mitikisiko ya kisiasa na kijamii katika baadhi ya sehemu ya nje ya bongo ambayo hufanya maisha kutokuwa ya salama sana kama ilivyo bongo.

Yote kwa yote, uamuzi wa kufanya kazi na kuishi nje ya bongo ni wa mtu binafsi kutegemeana na mpango wa maisha yake, na yote atakayokumbana nayo yanategemea mambo mengi ikiwa pamoja na nchi atakayokuwepo, aina ya kazi, kipato, nidhamu yake ya matumizi, na uwezo wake wa kujenga mahusiano na anaoishi nao.

Imeandikwa na Mdau,
SAUZI

0 comments: