MAMBO KAMA YALIVYO NJE YA TANZANIA

Thursday, 20 October 2011

KUTOFAHAMU SHERIA KULIVYOIAIBISHA BAFANA BAFANA

10:16 By Mindset

Taifa na dunia kwa ujumla ilishuhudia wachezaji na baadhi ya viongozi wa timu ya taifa ya Afrika Kusini - Bafana Bafana wakishangilia kutinga katika fainali za mataifa ya Afrika ya 2012 baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na timu ya taifa ya Sierra Leone.

Kwa mujibu wa tafsiri ya viongozi wa Bafana Bafana, kocha na hata baadhi ya wachambuzi wa soka hapa Sauzi, ni kuwa Bafana Bafana ilihitaji walau droo tuu kama timu ya taifa ya Misri ingeifunga timu ya Niger siku hiyo hiyo. Na kama ilivyotegemewa , timu ya Misri iliichapa timu ya taifa ya Niger mabao 3 kwa bila.

Na ndipo refa aliyecheza mechi ya Bafana Bafana na Sierra Leone alipopiga kipenga cha mwisho, uwanja mzima uligubikwa kwa furaha kuwa Bafana Bafana imepata tiketi ya kuenda kwenye fainali za mwaka 2012 za mataifa ya Afrika.  Hata hivyo masaa machache baada ya mechi hiyo taarifa zikaanza kusambaa kuwa Bafana Bafana haijapata ushindi kwani ilitakiwa kushinda siku hiyo, kwani pamoja na timu ya taifa ya Niger kufungwa na Misri, bado ilikuwa ina pointi nyingi na idadi kubwa ya ushindi ingawa Bafana Bafana ilikuwa ikiongoza kundi hilo.

Si ndipo uongozi wa chama cha mpira cha Sauzi - SAFA ukakata rufaa CAF kupinga Bafana Bafana kutopata tiketi ya fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2012, hata hivyo waziri wa michezo wa hapa aliwajia juu viongozi wa SAFA akisema kukata rufaa huko ni kuiabisha taifa na kwamba inabidi viongozi hao waliombe radhi taifa. Na akaongeza kuwa katika nchi nyingine viongozi kama hao hujiuzuru.

Viongozi wa SAFA siku ya Jumatano tarehe 19/10/2011 walitangaza rasmi kuondoa rufani yao CAF na kuliomba radhi taifa kwa aibu ya kutotambua vyema sheria za mashindano za CAF ,kwa maana hiyo wamekubali rasmi kuwa Bafana Bafana imekosa nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2012.

Hata hivyo SAFA imesema inafanya uchunguzi ilikuwaje viongozi wote wakashindwa kutambua kwa usahihi sheria ya Mashindano namba 14 ya CAF na kwamba kwa sasa hakuna kiongozi anayejiuzuru na kocha mkuu  Pitso Mosimane bado kibarua chake kinaendelea.

Na Mdau, Sauzi.

0 comments: